Mhe. Mchengerwa- Serikali yadhamiria kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili.
Na John Mapepele Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kujenga Chuo Kikuu cha Kiswahili ili kukuza na kubidhaisha lugha hii adhimu duniani. Mhe. Mchengerwa amesema haya leo, Januari 25, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akimkaribisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuhutubia kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo ya Kiswahili. Amesema, hivi sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazokua na kuenea kwa kasi kubwa ulimwenguni ambapo Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa kumi duniani. Hivyo, kasi ya ufunzaji na ujifunzaji wa lugha hii imekuwa ikiongezeka kila uchao. Aidha, amesema Kiswahili ni lugha ya mawasiliano mapana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwa upande wa Tanzania licha ya kuwa lugha ya Taifa ndiyo lugha kuu ya mawasiliano. Amefafanua kuwa lugha ya Kiswahili kwa sasa imevuka mawanda ya kuielezea lugha yenyewe na hivyo inatumika kuelezea taaluma mbalimbali kama vile afya,...