Misri kujenga viwanja changamani Dar, Dodoma, Mwanza na Arusha, yaahidi kutoa mafunzo maalum kwa waamuzi, makocha.

 

Na John Mapepele

Serikali ya Misri na Tanzania zimekubaliana kuimarisha mahusiano na mashirikiano kwenye  sekta ya  michezo kwa kujenga  miundombinu ya  michezo nchini na  kubadilishana  utaalam kwenye  michezo kwa faida ya pande zote mbili.

Hayo yamesemwa leo Agosti 18, 2022 na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa baada ya mkutano wa kujadili mambo mbalimbali ya kuimarisha michezo baina yake na Balozi wa Misri nchini Mhe. Mohamed Gaber Abulwafa.

Amesema Serikali ya Misri imekubali kujenga viwanja changamani vya michezo kwenye miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Arusha na Mwanza kwa gharama zao ambapo amesema viwanja hivyo vitakuwa vya kisasa ambavyo vitasaidia pia katika mashindano ya kimataifa.


Ameongeza kuwa mbali na kujenga viwanja vya michezo Serikali ya Misri imekubali kuisaidia Tanzania kwenye eneo la kutoa mafunzo kwa makocha na waamuzi wa soka ili wawe na viwango ambavyo vinakidhi   matakwa  ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA).

Aidha, amesema mafunzo hayo ya waamuzi yatasaidia katika kuwanoa waamuzi ili kupunguza malalamiko mbalimbali na kuendelea kulinda misingi ya nidhamu na maadili ya katika maeneo ya kupambana  na rushwa  pale wanapokuwa viwanjani. 

Ameongeza kuwa kwa sasa pande zote mbili zinakwenda kutekeleza mara moja makubaliano ambayo yalifikiwa Septemba 2021 na marais wa nchi zote  mbili kwenye eneo la michezo  kwa  faida ya  pande zote.


Comments