Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yashirikiana na Wizara ya Maliasili kuitangaza Tanzania, kukuza utalii.

 

Na John Mapepele

Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na Wizara ya Maliasili na Utalii leo Septemba 16 na  taasisi wadau wa Wizara hizo kutoka  pande zote za Muungano wamekutana na kufanya kikao  kujadili  namna bora ya kutumia Utamaduni, Sanaa na Michezo kukuza utalii.

Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Utamaduni,  Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa baada ya kikao hicho cha pamoja ambapo amefafanua kuwa wizara yake imekuwa na matukio makubwa ambayo yanauhusiano mkubwa  na Utalii.

Aidha, amesema kuna mambo ambayo wamekubaliana  kwa mshikamano na kutekeleza kwa pamoja  kuhakikisha kuwa sekta hizo zinakua.

Amesisitiza kuwa  Kwa Ushirikiano baina ya  wizara itasaidia kupeleka taifa  mbele kwa kuwa sekta hizo zinategemeana.

"Sisi katika Utamaduni tunao Utamaduni wa utalii, lakini katika michezo  kuna michezo na Utalii ambapo tunapokea wachezaji mbalimbali wa Kimataifa". Ameongeza  Mhe. Waziri

Amesema tayari taifa limeweza kupeleka timu nne za michezo mbalimbali kwenye kombe la dunia hivyo  kwa kushirikiana na  Wizara ya Utalii wanaweza  kuitangaza Tanzania Kimataifa.

Katika kikao hicho wamekubaliana kuwa na kalenda inayoonesha matukio yote  ya mwaka mzima ili kuweza kupanga namna bora ya kuuza utalii na kuondoka  na utalii wa msimu.

Pia mawaziri hao wameelekeza  watendaji  kukaa na kujadili kwa kina namna bora na mikakati ya kutumia sekta hizo kukuza  utali kabla kuwasilisha kwenye  vikao vya juu kwa maamuzi.

Kikao hicho pia kimefanyika kufuatia maelekezo  aliyoyatoa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Tamasha Utamaduni mjini Moshi ya kutaka Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia sekta hizo kuitangaza Tanzania na kukuza utali.


Comments